logo

WATALAAMU BMH WAPEWA MAFUNZO YA MAADILI KAZINI

Watalaamu mabingwa wa wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo wamepigwa msasa kwa kupatiwa mafunzo ya maadili katika semina ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.

Akitoa hotuba yake katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH na Mkurugenzi wa Upasuaji Dkt. Henry Humba amesema kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yatatolewa kwa awamu kwa madaktari wa Vitengo vingine pia na kusisitiza malengo yake ni kuboresha utumishi wa umma unaozingatia maadili.

"Malengo ya mafunzo hayo ya maadili kwa Madaktari Bingwa wa Upasuaji ni kuendelea kuwashirikisha maono ya Serikali ya kuhakikisha kuna kuwa na huduma bora kwa Wananchi kutoka kwa Watendaji na Wataalamu wa Serikali ambazo zimezingatia maadili ya Utumishi wa Umma" alisisitiza Dkt. Humba.

Dkt. Humba alitumia fursa ya mafunzo hayo.kuwajulisha Madaktari Bingwa wa Upasuaji (na Idara nyingine) kutambua kuwa uelekeo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa na hivyo inatakiwa kuwa na utamaduni unaokubalika na unaoendana na hadhi hiyo kubwa ikiwemo miiko ya kazi na maadili huku akiwatangazia Madaktari Bingwa wa Upasuaji juu ya Hatua za Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanzisha Kamati ya Usimamizi wa Vyumba vya Upasuaji (Theatre Committee).

"Lengo la kamati hii ya Usimamizi wa Vyumba vya Upasuaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (Theatre Committee) ni kuboresha na kuongeza kiwango cha utendaji wa mtumishi mmoja mmoja, ufanisi wa theatre zetu na Taasisi kwa ujumla, aidha kufanya ufuatiliaji na tathimin ya utekelezaji wa watumishi katika huduma za upasuaji na wote tunaohusika tushiriki ipasavyo" alisisitiza Dkt. Humba.

Nae Ndg. Salvatory Kaiza Mwezeshaji wa mada ya Maadili ya Utumishi wa Umma aligusia kuhusu taratibu, misingi na maadili ya utumishi wa Umma na kuwataka Madaktari hao kuvifuata kutokufanya hivyo kunaweza kuwasababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu na za kisheria.

"Kwa Mtumishi wa Umma kutotimiza Wajibu uliopangiwa na kutotimiza kwa ufasaha ni kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma, Madaktari wote ni lazima msimamie na kutekeleza Miongozo ya Madaktari na Viapo vya Madaktari mnavyoapa na kuzingatia maadili ya ujumla ya utumishi wa Umma, kutofanya hivyo unaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria" alikazia Ndg. Kaiza.

Aliongeza kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa iko katika mchakato wa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa, na kwa huduma zake wananchi wanatoka hadi mikoa mbalimbali hata yenye Hospitali kubwakubwa kama Dar es salaam kuja BMH kufuata huduma zake, lazima Madaktari na Watumishi wote kutoa huduma bora na kuzingatia maadili ili kulinda imani hiyo ya Wananchi walionayo juu ya BMH.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn